Kimenuka!
Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mafahari wawili wa Bongo Fleva, Ali
Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kudaiwa
kutupiana vijembe vya kufa mtu baada ya kuwepo kwa madai ya Kiba
kuhujumiwa.
Kwa
mujibu wa chanzo makini, ili kuweka hujuma ya kibiashara, hivi
karibuni, pamoja na kukanusha mara kadhaa kutokuwa na tatizo na Kiba,
Diamond alidaiwa ‘kutengeneza’ kwa makusudi penzi la mwigizaji
Jacqueline Wolper Massawe na msanii wa Wasafi Classic Baby (WCB), Rajabu
Abdulhan ‘Harmonize’ kisha kuvujisha video ya uhusiano huo mpya siku
ambayo Kiba alikuwa akiuachia wimbo wake mpya wa Aje (Jumamosi
iliyopita), lengo likiwa kuhamisha upepo mashabiki kutoka kwenye wimbo
mpya na kujali mapenzi ya wawili hao.
“Ni
hujuma ya kibiashara, Diamond na uongozi wake wameamua kumfanyia Kiba
ili wimbo wake ukose kiki kwa watu,” kilidai chanzo chetu.
VIJEMBE VYATAWALA
Hata
hivyo, kwa mujibu wa mmoja wa mameneja wa Kiba ambaye hakupenda jina
lichorwe gazetini, amemtupia vijembe Diamond kwa kudai licha ya hujuma
hizo lakini hawawezi kumgusa Kiba.
“Wanajisumbua,
kizuri huwa kinajiuza chenyewe na huwezi kuzuia mafuriko kwa mikono.
Wameingiza kiki zao lakini msimu huu hazifui dafu. Wimbo (Aje)
umepokelewa vizuri na una mafanikio makubwa hadi sasa.
AZUNGUMZIA MKATABA
“Kuonesha
kwamba Kiba amekubalika, ndani ya muda mfupi baada ya wimbo huo kuruka
hewani, amelamba mkataba na kampuni ya kimataifa ya Sonny Music. Sasa
hapo ndipo utakapoona Ngoma ya Kiba imekubalika kiasi gani, hawamuwezi
huyu,” alisema meneja huyo.
KEJELI SASA!
Kama
hiyo haitoshi, meneja huyo alizidi kutupa vijembe kwa Diamond kwa
kueleza kuwa Kiba ni mkongwe hivyo kamwe hawezi kulingana naye kimuziki.
“Diamond
hamuwezi Kiba, ameanza kuimba wakati Diamond bado hajawa msanii.
Ameshafanya mengi kwenye huu muziki kuliko huyo Diamond, unakumbuka dili
la One 8, Kiba aliungana na mastaa wakubwa katika project iliyokuwa
chini ya msanii mkali duniani, R-Kelly (Robert Sylvester Kelly),
Watanzania wanajua,” alisema meneja huyo.
KIBA HUYU HAPA
Alipoulizwa
Kiba kuhusiana na vijembe na kejeli hizo anazodaiwa kuzitupa kwa
mpinzani wake (Diamond), alisema ishu hiyo isiitwe vijembe badala yake
ieleweke kwamba ndiyo ukweli.
“Siyo vijembe wala majungu. Huo uliosikia ndiyo ukweli wenyewe,” alisema Kiba.
TEAM DIAMOND WAJIBU MAPIGO
Kupitia
mitandao mbalimbali ya kijamii, wafuasi wa Diamond waliojipa jina la
Team Diamond walicharuka kusikia msanii wao amehusishwa na hujuma za
‘kumuua’ Kiba kibiashara.
“Hana
lolote huyo, Diamond ameshafanya makubwa sana ndani ya muda mfupi
kumzidi yeye ndiyo maana anatapatapa kwa sababu nani asiyejua kuwa
Diamond yupo fasta katika kuona fursa kuliko Kiba?
“Wolper
na Harmonize wapo penzini kwa matakwa yao na si kwa kumuua Kiba, hana
jipya,” aliandika mmoja wa wafuasi wa Diamond kwenye Mtandao wa Kijamii
wa Instagram.
DIAMOND ANASEMAJE?
Jitihada
za kumpata Diamond ili azungumzie suala hilo hazikuzaa matunda kufuatia
simu yake ya mkononi kutopatikana hewani hadi tunakwenda mitamboni
lakini meneja wake, Babu Tale alipoulizwa kuhusu suala hilo, alicharuka:
Risasi
Jumamosi: Tale tuambie, hivi kuna ukweli wowote kwamba Diamond na timu
yako mlipanga kumzima Kiba alipokuwa anatambulisha ngoma yake mpya kwa
kutupia video inayoonesha uhusiano wa Wolper na Harmonize?
Tale:
“Siyo kweli. Hilo swali ni la kipuuzi. Sikiliza, ngoja nikuunganishe na
bosi wako ili asikie unavyoniuliza. Nakata halafu nakupigia.
Hata hivyo, Babu Tale hakufanya hivyo na alipopigiwa tena, simu yake haikupatikana.
WOLPER AFUNGUKA
Gazeti
hili halikuishia hapo, lilimtafuta Wolper ili kujua kama ni kweli
ametumika kumfifisha Kiba kimuziki ambapo alisema si kweli kwani penzi
lake na Harmonize limetoka katika mioyo yao.
“Hakuna
kitu kama hicho. Sisi tumependana wenyewe wala hatujashinikizwa na mtu
yeyote kuvujisha penzi letu eti ili kumfanya fulani afifie! Kama
imetokea limevuja wakati ambao huyo Kiba naye ametoa wimbo itakuwa tu
imetokea lakini si kwamba tumedhamiria,” alisema Wolper huku simu ya
Harmonize ikiita bila kupokelewa.
Ugomvi
wa Diamond na Kiba ni wa muda mrefu ambapo huwa na msimu kwani kuna
wakati unachachamaa kama sasa na kipindi kingine unapoa na hakuna
anayejua hatima yao.
Chanzo: Global Publishers
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment