KIKI siyo kitu kigeni kabisa kwa wasanii ulimwenguni. Kutafuta jambo la
kushtua na kuwafanya mashabiki wamzungumzie msanii husika kwa muda mrefu
zaidi akiwa na lengo la kuachia kazi yake.
Lakini kwa baadhi ya wasanii wetu hapa Bongo hujiingiza kwenye skendo
wakidhani ni kiki. Kwa kawaida kiki ni nzuri ili kumsaidia msanii
kujipaisha na kuchomoa kazi yake, lakini si kwa kujiharibia kwa kashfa
mbaya ambazo mwisho wake kufutika inakuwa shida.
Yes! Hapa Bongo wapo mastaa wengi ambao wametingisha kwa kiki huku
wengine wakijaribujaribu. Polisi wa Swaggaz anakudondoshea kiki za
mastaa zilizotingisha zaidi tangu kuanza kwa mwaka huu.
RUBY, ASLAY
Kila mtu aliongea lake ilipovuma kuwa Ruby anatoka na Aslay ambaye
kiumri ni mdogo kwake. Hii ilitokea Juni 13, mwaka huu mara baada ya
Ruby kuanza kutupia picha za Aslay kwa fujo kwenye ukurasa wake wa
Instagram na kuandika meneno yanayoashiria kuna mahaba mazito kati yao.
Aslay yeye alimjibu Ruby kwa jumbe tamu za mahaba na kuzidi
kuwachanganya mashabiki huku wengi wakitamani kuona kama penzi hilo
jipya mjini litakuwa na uzito wa kuipiku kapo ya Harmonize na Wolper
iliyokuwa inatamba kipindi hicho.
Wakati watu wengi wanazidi kumiminika na kuifuatilia kapo hii ndipo
Yamoto Band wakaachia ngoma yao mpya inayoitwa Suu, waliyomshirikisha
Ruby.
Ikasanuka kumbe ilikuwa kiki tu. Hilo lilithibitishwa hata na meneja wao Said Fella ‘Mkubwa Fella’ a.k.a Mheshimiwa Diwani.
LINEX
“Ahsante Mungu, kuna maamuzi hayahitaji matangazo, silence speaks
volumes,” aliandika Linex kwenye ukurasa wake wa Instagram mara baada
ya kutupia picha akiwa kwenye mikao tofauti na mrembo aliyedai kuwa
amemuoa.
Linex alizidi kupokea pongezi kutoka kwa mashabiki waliovutiwa na tukio
la yeye kufunga ndoa, uamuzi ambao ni nadra mno kwa wasanii wa Bongo
Fleva.
Hali ilikuwa tofauti mara baada ya kutumia picha zilezile za harusi
kutengeneza kava la ngoma yake mpya iitwayo Kwa Hela, aliyoachia
mwanzoni mwa mwaka huu.
Kwa tukio hilo, Linex alijikuta akipokea matusi kutoka kwa mashabiki kwa
kosa la kuchezea hisia zao lakini mbali na kadhia hiyo lengo lake la
kutumia Kiki lilifanikiwa, aliapoachia ngoma yake ikapenya.
RAY KIGOSI
Vincent Kigosi ‘Ray’ alifanikiwa kuwakamata mashabiki wake kwa
kutengeneza kiki yenye ‘akili’ sana. Yeye aliibuka na maelezo kuwa weupe
wake ni kwa sababu anatumia maji mengi na kushiriki mazoezi.
Ray alisema hayo wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga jijini Dar
es Saalam. Hakuna kiki inayofikia hii tangu mwaka huu umeanza. Katika
mitandano ya kijamii watu mbalimbali walipiga picha wakiwa wanakunywa
wakidai wanataka kuwa weupe kama Ray!
Ile kushangaashangaa, Ray akaachia Filamu ya Tajiri Mfupi ambayo
ilifanya vizuri sokoni. Pamoja na kiki hiyo, Tajiri Mfupi ni kati ya
sinema bora za Kibongo zilizotoka mwaka huu.
VANESSA MDEE
“Nikupe Kiki ujulikane au siyo? Kila siku twanyamaza ndiyo mtugaragaze.
Mimi siyo wale uliowazoea,” aliandika Vanessa Mdee kwenye instagram
akimshambulia Shilole.
Shilole hakukaa kimya naye kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika:
“Veepe jipange sana, mwenzio Igunga niliaga, sijaletwa kwa kubebwa
kwenye lori, nimekuja na mbio za mwenge. We si wa magorofani na
kiingereza chako cha kuunga mi ndo mtoto wa mbwa, sasa ole wako tukutane
utanyooka.”
Watu wakahamishia mawazo yao kwao, kutahamaki kumbe walikuwa wanaandaa
shoo Club Bilicanas, Dar. Shoo ilikuwa poa kutokana na kiki hiyo.
NEDY MUSIC
Baada ya Shilole kumwagana na Nuh Mziwanda watu walikuwa wanatamani
kufahamu ni nani ataziba pengo hilo. Ghafla kijana mdogo Nedy Music
akaanza kuhisiwa kutoka kimapenzi na mwanadada huyo.
Sababu kubwa iliyofanya watu waanze kuhisi kuwa kuna penzi kati yao ni
picha walizokuwa wanatupia kwenye Instagram zikiambatana na maneno ya
mapenzi.
Hakuna aliyemjua Nedy Music kabla ya kuwa na Shilole lakini alipata
umaarufu mara baada ya kiki hiyo ya kumrithi Nuh Mziwanda, hata
alipoachia ngoma yake Usiende Mbali chini ya Ommy Dimpoz kupitia lebo
ya PKP alichomoka kirahisi tu.
Na hapo ndipo ikajulikana kuwa hakukuwa na mapenzi kati yao bali ilikuwa
kiki ya kutafuta mashabiki kwenye muziki huu wenye ushindani. Kwa hilo
alifanikiwa.
Sunday, July 10, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment