Mtanzania Mbwana Samatta aliweka rekodi ya kufunga katika michuano ya
Europa League baada ya timu yake ya Genk kuibuka na ushindi wa magoli
2-0 mbele ya Budućnost ya Montenegro.
Clouds FM kupitia kipindi chake cha michezo cha Sports Extra kilifanya
mahojiano maalu na Samatta kutaka kujua mambo mbalimbali. Mtandao huu
ukaona haitakuwa vibaya kama utakuletea kile alichokisema nyota huyo
hasa kama ulikosa kusikiliza show ya Sports Extra.
sportsextra: Mbwana Samatta unajisikiaje kuwa Mtanzania wa kwanza kufunga goli katika michuano ya Europa League?
Samatta: Nimejisikia vizuri kwasababu ndiyo kitu ambacho kila
siku nakipigania kuweza kufanikiwa, mshambuliaji unaweza kufunga magoli,
nimejisikia vizuri na inanipa morali zaidi ya kuendelea kujituma.
sportsextra: Ulianza katika kikosi cha kwanza mbele ya Nikola
Karelis mshambuliaji wa kutumainiwa wa Genk, hii inamaanisha kuwa
mwalimu Peter Maes anakuamini sana kuliko mshambuliaji huyo
anayehusishwa na kujiunga na klabu ya Nottingham Forest ya nchini
England?
Samatta: Nafikiri sasahivi mwalimu ananiamini na anapenda
kunitumia, ni kitu ambacho kwakweli ni kizuri kwangu mwenyewe binafsi
lakini pia nafikiri yeye kwake anaona namsaada mkubwa kwenye timu yake
nikiwa naanza kwenye kikosi cha kwanza. Nafikiri ni jambo la kusubiri
muda utakapofika kilakitu kitakuwa wazi lakini kwa sasahivi nafikiri
mwalimu anapenda kunitumia zaidi.
sportsextra: Watu wengi walikuwa wanajaribu kujiuliza kuwa Mbwana
yupo wapi wakati wa likizo yako baada ya kusimama kwa Ligi Kuu ya soka
nchini Ubelgiji. Watu wanataka kujua ulikuwa wapi Mbwana wakati wa
mapumziko?
Samatta: Likizo nilikuwa Tanzania japo likizo ilikuwa fupi lakini
nilikuwa nyumbani nimepumzika ilikuwa ni kipindi cha mwezi wa Ramadhani
kwahiyo nilikuwa kwenye mfungo. Ilikuwa haina sababu ya kuonekana
kwasababu ilikuwa ni kipindi cha mapumziko.
Ukifata program ya mazoezi kutoka kwenye timu, ilikuwa ni muda wa
kupumzika kwa wiki moja halafu wiki nyingine unatakiwa ufanye mazoezi
wewe mwenyewe binafsi. Lakini kwa bahati mbaya mimi sikupata muda wa
kupumzika kwasababu wakati likizo inaanza mimi nilitakiwa nijiunge na
timu ya taifa kwa ajili ya mechi dhidi ya Misri na baada ya hapo
niliendelea na program ambayo nilipewa mimi binafsi.
Mchezaji anapopewa likizo anatakiwa apumzike kabisa kwasababu ni kipindi
ambacho mwili wake unatakiwa ujirudi na kutengeneza nguvu mpya. Haina
maana kwamba ukipewa likizo basi ujifue na kujiweka nondo hapana, muda
wa mapumziko ni kipindi ambacho anatakiwa apumzike kama amepewa program
basi afanye lakini asijichoshe.
sportsextra: Mbwana nafasi ya timu yako ya Genk sasa unaionaje
katika michuano ya Europa League baada ya jana kupata ushindi mbele ya
klabu ya Budućnost?
Samatta: Nafikiri bado tunakibarua kwasababu ni mechi ya kwanza
na tumeshinda kwa goli 2-0, mpinzani sasahivi kichwani kwake anajua
kwamba amefungwa goli mbili na anahitaji kurudisha na kupata ushindi
akiwa nyumbani, kwahiyo kibarua bado kipo siwezi kusema moja kwa moja
kwamba tutakata tiketi ya kucheza kwenye makundi lakini nafikiri tuna
timu nzuri na tunaweza kufika huko kwa hiyo kila kitu ni wakati.
sportsextra: Asante sana Mbwana Samatta.
Monday, July 18, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment